Kwa habari zaidi kuhusu ORBIT tembelea tovuti ya: www.orbit-tz.com
KWA MAONI AU USHAURI TUTUMIE KWENYE E-mail: kusinileo@gmail.com

Thursday 16 June 2016

PROF MBARAWA ATETA NA BODI MPYA BANDARI

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) Prof. Ignas Rubaratuka (wa pili kulia) akijadiliana jambo na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani) kwa njia ya teknolojia ya video (Video Conference) katika kikao kazi kati ya Waziri na Bodi hiyo. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu, Sekta ya Uchukuzi Dr. Leonard Chamuriho.Picha na Ofisi ya Waziri

Kikao kazi cha Bodi Mpya ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani), Kikao hicho kimefanyika kwa njia ya teknolojia ya video (Video Conference). Bodi ikiwa jijini Dar es Salaam na Waziri na Naibu wake wakiwa mjini Dodoma.Picha na Ofisi ya Waziri


Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuanza kazi mara moja kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili Mamlaka hiyo hapa nchini.
Akizungumza na bodi hiyo kupitia Teknolojia ya Video (Video Conference) toka mjini Dodoma Prof. Mbarawa ameitaka bodi hiyo kufahamu kuwa miundombinu ya banadri nchini iko katika hali duni, isiyo uwiana na malengo ya Serikali ya kuwa na bandari itakayoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Kazi yenu kubwa ya kwanza ni kurudisha uadilifu na ufanyakazi wa uzalendo na unaozingatia weledi kwa watumishi wote wa bandari nchini”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesema TPA inakabiliwa na changamoto nyingi  zikiwemo watu kuajiriana kindugu, utendaji usiozingatia matokeo, mifumo mibovu ya ukusanyaji mapato, baadhi ya watendaji kuwa na maslahi binafsi katika kampuni zinazofanya kazi bandarini na utendaji dhaifu wa matumizi ya mifumo ya elektoniki hali inayosababisha utendaji usio na ufanisi.
Aidha Prof. Mbarawa amezungumzia umuhimu wa bodi hiyo kuangalia upya muundo wa bodi ya zabuni ya bandari na namna kampuni zinazopewa zabuni zinavyopatikana ili kuondoa manung’uniko na mikwamo katika utekelezaji wa miradi.
“Hakikisheni mnaweka watu waadilifu, wasio na maslahi binafsi katika bodi za zabuni ili kuiwezesha bandari kushindana na bandari za nchi nyingine na hivyo kuvutia wasafirishaji wengi hali itakayoongeza mapato ya bandari na  kukuza uchumi wa nchi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TPA Prof. Ignas Rubaratuka amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kubadili changamoto zote za bandari nchini kuwa fursa na kazi hiyo itafanywa kwa weledi na kwa muda mfupi.
Amesema watahakikisha kuwa malalamiko yanayotokana na bandari yanashughulikiwa kwa weledi na kwa kufuata sheria ili haki itendeke na kuiwezesha  bandari kuwa na hadhi inayostahili.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho ameitaka bodi hiyo kujifunza majukumu yake kwa haraka na kutenda kazi kwa mujibu wa sheria.
Bodi Mpya ya Bandari nchini ambayo imeanza kazi rasmi Juni 14, 2016 inatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na inaundwa na  wajumbe nane ambao ni Mwenyekiti Prof. Ignas Rubaratuka, Dkt. Jabir Bakari, Bw. Azizi Kilonge, Eng. Deusdedit  Kakoko, Bw. Masanja Kadogosa, Bw. Japhary Machano, Bw. Malata Pascal, Dr. Francis Michael na Bi Jayne Nyimbo

No comments:

Post a Comment