Kwa habari zaidi kuhusu ORBIT tembelea tovuti ya: www.orbit-tz.com
KWA MAONI AU USHAURI TUTUMIE KWENYE E-mail: kusinileo@gmail.com

Thursday 27 March 2014


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya mwaka 2012/2013 na mwaka 2013/2014, Waziri wa Nishati na Madini alitoa wito kwa wamiliki wa leseni za madini kuwataka kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Aidha, Waziri alitamka bayana kuwa wale wote watakaobainika kukiuka sheria  na masharti ya leseni zao wangefutiwa leseni.

Katika kutekeleza agizo hilo, wamiliki wa leseni 888 walipewa notisi za makosa katika kipindi cha mwaka 2012/2013; ambapo jumla ya leseni 160 za utafutaji na leseni moja ya uchimbaji wa kati zilifutwa. Aidha, leseni 268 za uchimbaji mdogo zilifutwa.  Kwa kipindi cha mwaka 2013/2014, wamiliki wa leseni 289 walipewa notisi za makosa. Kati ya leseni hizo, 211 zilikuwa za utafutaji mkubwa wa madini, leseni 78 zilikuwa za uchimbaji wa kati na leseni moja ya uchimbaji mkubwa wa madini ya makaa ya mawe katika eneo la Kabulo. Kutokana na taarifa hizo za makosa, jumla ya leseni 174 za utafutaji madini na leseni moja ya uchimbaji mkubwa zimefutwa kwa mujibu wa sheria.

Wizara hivi sasa imeunda Timu Maalum ya ukaguzi ambayo inatembelea maeneo yote ya utafutaji na uchimbaji wa madini, pamoja na maduka ya wafanyabiashara wa madini nchini ili kujiridhisha kama wahusika wanatimiza masharti ya leseni walizopewa. Timu hiyo imeanza kazi yake kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara na itaendelea na kazi hiyo katika maeneo yote nchini. Wale wote watakaobainika kukiuka masharti ya leseni, watapewa hati za makosa na leseni zao kufutwa iwapo watashindwa kurekebisha kasoro hizo.

Pamoja na hatua hizo, Wizara pia imeanza kudhibiti umilikaji wa maeneo makubwa ya leseni kwa kutowapa maeneo mapya wale ambao maeneo wanayoyamiliki hivi sasa yanazidi kilomita za mraba 2,000. Pia, Wizara  inaendelea kufuta leseni ambazo maeneo yake hayafanyiwi kazi na wamiliki wake.  

Tanzania imejaliwa hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali ambayo imevutia watu na kampuni nyingi kuomba leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini. Umilikaji wa leseni za madini hapa nchini unaongozwa na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake.

Kutokana na mvuto wa uwekezaji uliopo katika sekta ya madini, hadi sasa kuna jumla ya leseni 3,950 za utafutaji mkubwa wa madini, pamoja na maombi 3,677 ya leseni hizo. Aidha, kuna leseni 393 za uchimbaji madini wa kati na maombi 99 ya leseni za uchimbaji. Leseni za uchimbaji mdogo hadi sasa zinafikia jumla ya 35,717 na maombi 16,263.

Pamoja na uwingi huo wa leseni za madini, imebainika kuwa baadhi ya wamiliki wa leseni wanakiuka sheria ya madini kwa kuhodhi maeneo makubwa ya leseni, kukwepa kulipa ada, mrabaha na kodi kwa wakati na ama kushikilia maeneo yaliyo chini ya leseni zao bila kuyafanyia kazi. Hali hii inachelewesha ukuaji wa sekta, na kuikosesha Serikali mapato. Ni azma ya Wizara kuhakikisha kwamba speculators wote wanaachia maeneo wanayoyashikilia hivi sasa ili wawekezaji walio tayari kuyaendeleza wamilikishwe.

Tunapenda kuwaomba wamiliki wa leseni za madini kuzingatia wajibu wa kuyaendeleza maeneo ya leseni walizomilikishwa na Wizara ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mhandisi Paul M. Masanja
KAMISHNA WA MADINI


No comments:

Post a Comment