Kikao kazi cha Bodi
Mpya ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Waziri na Naibu Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani), Kikao hicho kimefanyika
kwa njia ya teknolojia ya video (Video Conference). Bodi ikiwa jijini Dar es
Salaam na Waziri na Naibu wake wakiwa mjini Dodoma.Picha na Ofisi ya Waziri
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Usimamizi
wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuanza kazi mara moja kwa kuzipatia
ufumbuzi changamoto zinazoikabili Mamlaka hiyo hapa nchini.
Akizungumza na bodi
hiyo kupitia Teknolojia ya Video (Video Conference) toka mjini Dodoma Prof.
Mbarawa ameitaka bodi hiyo kufahamu kuwa miundombinu ya banadri nchini iko
katika hali duni, isiyo uwiana na malengo ya Serikali ya kuwa na bandari
itakayoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Kazi yenu kubwa ya
kwanza ni kurudisha uadilifu na ufanyakazi wa uzalendo na unaozingatia weledi
kwa watumishi wote wa bandari nchini”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesema TPA inakabiliwa
na changamoto nyingi zikiwemo watu
kuajiriana kindugu, utendaji usiozingatia matokeo, mifumo mibovu ya ukusanyaji
mapato, baadhi ya watendaji kuwa na maslahi binafsi katika kampuni zinazofanya
kazi bandarini na utendaji dhaifu wa matumizi ya mifumo ya elektoniki hali
inayosababisha utendaji usio na ufanisi.
Aidha Prof. Mbarawa
amezungumzia umuhimu wa bodi hiyo kuangalia upya muundo wa bodi ya zabuni ya
bandari na namna kampuni zinazopewa zabuni zinavyopatikana ili kuondoa
manung’uniko na mikwamo katika utekelezaji wa miradi.
“Hakikisheni mnaweka
watu waadilifu, wasio na maslahi binafsi katika bodi za zabuni ili kuiwezesha
bandari kushindana na bandari za nchi nyingine na hivyo kuvutia wasafirishaji
wengi hali itakayoongeza mapato ya bandari na
kukuza uchumi wa nchi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TPA Prof. Ignas Rubaratuka amemhakikishia Waziri
Prof. Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kubadili changamoto zote za bandari nchini
kuwa fursa na kazi hiyo itafanywa kwa weledi na kwa muda mfupi.
Amesema watahakikisha
kuwa malalamiko yanayotokana na bandari yanashughulikiwa kwa weledi na kwa
kufuata sheria ili haki itendeke na kuiwezesha
bandari kuwa na hadhi inayostahili.
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard
Chamuriho ameitaka bodi hiyo kujifunza majukumu yake kwa haraka na kutenda kazi
kwa mujibu wa sheria.
Bodi Mpya ya Bandari
nchini ambayo imeanza kazi rasmi Juni 14, 2016 inatarajiwa kudumu kwa kipindi
cha miaka mitatu na inaundwa na wajumbe
nane ambao ni Mwenyekiti Prof. Ignas Rubaratuka, Dkt. Jabir Bakari, Bw. Azizi
Kilonge, Eng. Deusdedit Kakoko, Bw.
Masanja Kadogosa, Bw. Japhary Machano, Bw. Malata Pascal, Dr. Francis Michael
na Bi Jayne Nyimbo
|
No comments:
Post a Comment